Tuesday, March 29, 2011

makala-maisha ya gerezani na uozo unaofukuta Na.3


Na Thompson Mpanji

......Japokuwa kwa mujibu wa maelezo ya wafungwa waliokaa kwa muda mrefu wakitumikia vifungo vyao wamekuwa wakisema  kuwa kwa miaka ya hivi karibuni kuna mabadiliko makubwa ya uangalizi na utunzaji wa mahabusu na wafungwa, lakini kwa upande wangu bado haikuniingia akilini baada ya kushuhudia mara kadhaa watu wakipigwa virungu kama mbwa mwizi.

Vitendo hivyo vimekuwa vikifanyika mara nyingi na maaskari wenye vyeo kuanzia staff sajenti kushuka chini( wasiokuwa na vyeo),nimeshuhudia laivu mara kadhaa askari anayeshughulika na mambo ya jikoni mwenye cheo cha sajenti maarufu kwa jina la gerezani kama mchokocho amekuwa akidiriki hata kuwapiga watu kwa kutumia mawe na vikombe bila kujali madhara yatakayotokea.

Vitendo hivyo vya upigaji ovy vimekuwa vikifanywa hata na wafungwa kuwapiga mahabusu jambao ambalo linafanywa ni la kawaida.

Tukiachana na virungu tunakutana na pointi  ya mizinga ,hii sehemu ni maarufu kwa ajili ya kukagua watu wanaoingia ama kutoka kwa kuamriwa kuvua nguo zote na kulazimishwa kuinama na kupanua makalio.

Zoezi hili limekuwa likifanywa kila kukicha bila kujali umri na wala haizingatiwi kama kuna baba na mtoto au mkwe hali inayoonyesha kuwa ni sehemu ya kudhalilishwa.

Imefikia wakati hata nguo mnazovaa ambazo ni safi zinatupwa chini na kukanyagwa kanyagwa ovyo na kuonekana hazina thamani yeyote na hauruhusiwi kusema lolote kinachotakiwa ni kufyata mkia.

Kwa ujumla utu  wa mtu ndani ya gereza unachukuliwa kuwa hauna thamani yeyote na kwamba kwa vile umeshakuwa mahabusu au mfungwa basi hauna haki ya kulalamika chochote zaidi ya ndiyo ‘bwana mkubwa’.

Hata unapoongea na askari hautakiwi kusimama nilazima uchuchumae hata ikiwa mtaongea masaa mawili bila kujali kama unaumia au umechoka.

Kwa ujumla jeshi la magereza bado linatumia  sheria na taratibu za kikoloni ambazo baadhi yake zimepitwa na wakati na hivyo kunahitajika mabadiliko yanayokwenda na wakati.

Ukiangalia vitendo vya manyanyaso na udhalilishaji vinavyofanyika kwa mahabusu kwa mahabusu au wafungwa kwa mahabusu hasa wakati wakutembelewa na ndugu vimekithiri.

Utakuta mfungwa anampiga mahabusu na kumkunja na kumsukuma sukuma huku ndugu yake akiwa anamwangalia na huku askari akisaidia unyanyasaji huo badala ya kukemea.

Ofisi ya utawala ndiyo ofisi kuu ya kufika na kusajiriwa na ndiyo ofisi inayotumika katika  kutoka lakini ofisi hiyo imekuwa ikiwafukuza watu kabla hata haujatoa shida yako imekuwa ni ofisi ya kuogopwa badala ya kukimbiliwa.

Admission ndiyo ofisi ya kuingilia na kutokea gerezani na ndiyo ofisi inayosikiliza matatizo yote ya mahabusu na wafungwa kabla ya kufika kwa Mkuu wa gereza  lakini haipo hivyo,wanabainisha wafungwa na maabusu ambao wamekuwa wakilalamika muda wote.

Pia kuna suala moja ambalo ni hatari sana ingawa linachukuliwa ni la kawaida lakini naamini ipo siku litakuja kuleta madhara makubwa kama wasemavyo waungwana ‘mzaa mzaa uzaa usaa’.

Mimi nakumbuka siku niliyokuwa natolewa polisi kituo cha kati kilichopo Mkoani hapa na kuingia ndani ya lori kubwa la kuchukuwa mahabusu maarufu kama karandinga tuliambiwa na polisi waliokuwa wakitulinda kuwa kama tunazo fedha tukabidhi maana huko tunakoenda kuna majambazi watakaotupiga ,kutukaba na kutunyang’anya fedha.

Nilijiuliza hao majambazi watatoka wapi ilhali tupo na maaskari,sikupata jibu na kwa vile sikuwa na kitu chochote chenye thamani sikuhofu.

Basi baada ya kuondoka hapo kituoni tulipitia magereza kuwachukuwa mahabusu waliokuwa wanakwenda mahakamani.

Alianza kuingia mahabusu mmoja baada ya mwingine na hapo walianza kutuangalia usoni na ghafla nikakuta wenzangu wanakabwa na kuanza kukaguliwa huku wakiambiwa kama una fedha toa wewe mwenyewe bila kupigwa.

Kwa kweli hali ile ilinishtusha sana na kuona mambo haya yamekuwa tuumachi yaani watu wanakabwa huku polisi wanaona na wasichukue hatua yeyote inashangaza na kusikitisha na iwapo hali ndiyo hiyo je huko mitaani haiwezekani polisi hawa hawa wakashirikiana na hao waharifu kufanya uharifu?.

Kama kwamba haitoshi baada ya kufika katika lock up iliyopo mahakamani hali ndiyo ilizidi kuwa mbaya zaidi baada ya wale vijana niliotoka nao Central kuanza kupigwa na kukabwa kooni huku wakilazimishwa waonyeshe walipoficha fedha.

Vijana hao walipiga mayowe ya kuomba msaada kwa askari bila mafanikio hadi sauti zilipowaishia kwa kukabwa kupita kiasi hadi hao wanyang’anyi walipomaliza kazi yao na kuwaacha vijana wakiwa hoi bin taaban.

Ukweli hali hiyo isipodhibitiwa watu wanaweza wakauana na nina kumbuka imeshawahi kutokea mahabusu kadhaa kupewa adhabu baada ya kufanya mchezo huo wakati karandinga halijatoka magereza.

Pia kuna mahabusu waliowahi kushtakiwa  katika mahakama ya wilaya kwa makosa ya kupaka kinyesi,kupiga na kujeruhi mahabusu wenzao.

Kutokana na hali hii  nina amini mamlaka pamoja na taasisi husika na masuala ya mahabusu na wafungwa zitafuatilia, kurekebisha  na kuboresha yale yanayowezekana kama ambavyo Mkuu wa gereza la Ruanda anavyodaiwa kurekebisha vifo vya mahabusu na wafungwa vilivyokuwa vikitokea kabla hajaanza kuongoza gereza hilo.

Aidha Jesh la magereza imefika wakati wa kurekebisha sheria na taratibu zilizopitwa na wakati na kuendelea kuimarisha mfumo wa mafunzo kwa wafungwa badala ya kuwa mfumo wa mateso ili mfungwa akimaliza kutumikia adhabu yake aende akawe raia mwema na mfano wa kuigwa katika jamii.

Hata hivyo katika makala ya mwisho   mwandishi wa makala haya atafanya mahojiano  maalum na Mkuu wa Magereza Mbeya,Kamanda wa Jeshi la polisi Mbeya,Hakimu mkazi Mkoa,Mwanasheria mkuu,msajili wa mahakama,Asasi zinazoshughulika na masuala ya haki za binadamu na sheria,Magereza mengine,Idara ya Ustawi wa jamii na baadhi ya wafungwa na mahabusu ili kujuwa hali ilivyo sasa na jitihada za kubadilisha hali za maisha ya wafungwa na mahabusu magerezani.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment