Tuesday, March 29, 2011

makala-maisha ya gerezani na uozo unaofukuta Na.2


Na Thompson Mpanji
......Wanafunzi hao waliendelea kusema kuwa lakini walibahatika kuhama katika chumba hicho namba 12 na  kuhamia chumba namba saba ambapo walimkuta ndugu yao ambaye aliwasaidia kwa kiasi kikubwa kuepuka balaa hilo.

Hata hivyo Vijana hao waliiomba serikali kuzingatia kuwatenganisha watoto na watu wazima  na kwamba suala la kuwatenga katika chumba namba tano cha kulala watoto wadogo ndani Gereza hilo bado halisaidii chochote.

Pia wamewaomba wazazi kujaribu kutafuta njia nyingine mbadala itakayoweza kuwaadhibu ama kuwaonya watoto kuacha vitendo vya uharifu kuliko kuwapeleka magerezani hali inayopelekea kulawitiwa na kuambukizwa ugonjwa wa Ukimwi.

Vile vile wameiomba Serikali ibuni adhabu za kuwatia adabu kwa kuwaadhibu,udhibiti wa kijamii na makazi ya mpito ambapo wahalifu wadogo wawekwe na kupewa ushauri nasaha na huduma ya adhabu ya jamii.

Aidha Vijana hao wamewataka vijana kuacha tabia ya uharifu kwani madhara yake  ni makubwa baada ya kufikishwa gerezani kwani watashindwa kuhimiri misuko suko ya jela na hivyo watalawitiwa na kuambukizwa Ukimwi na hatmaye kupoteza maisha.

Tume ya Jaji Kisanga katika taarifa yake ya uchunguzi Magerezani iliyotolewa na idhaa ya kiswahili ya BBC mnamo April,19.mwaka huu ilithibitisha kuwepo kwa mlundamano na kutotenganishwa vijana chini ya miaka 18 hali inayochangia kuwepo kwa vitendo vya kujamiiana.

Hata hivyo imebainika kuwa asilimia kubwa ya watu ‘wanaocheza’mchezo huo wanakuwa wamefanyiwa mchezo huo kwa hali hiyo nao wanakuwa  na dhana ya kulipiza na kwamba mara kadhaa watu huwa wanarubuniwa siku ya kwanza waingiapo Gerezani.

Pia uchunguzi huo umebaini kuwa  asilimia 85% ya manyapara wa kifungwa ni wachezaji wa mchezo huo mchafu na hivyo inakuwa vigumu suala hilo kulidhibiti na kutokana na ushirikiano wao wa kutenda madhambi hayo inakuwa ni vigumu kesi za namna hiyo kufika kwa Mkuu wa Gereza.

Mara kadhaa kesi za namna hiyo zinaishia kushindwa kwa mtendewa kosa kwa kuonekana ni muongo mwenye nia ya kutaka kumuharibia cheo nyapara fulani na hivyo mlalamikaji uishia kupigwa virungu na kutokana na maaskari wengi kuwasikiliza hao manyapara basi wanaotendewa uishia kunun’gunika kimya kimya siku zote.

Pamoja na kukithiri kwa vitemdo hivyo lakini pia kuna jitihada za chini chini zinazofanyika katika kujaribu kukemea matendo hayo kama ambavyo Mwalimu mmoja wa dini wa kanisa la katoliki ndani ya Gereza ambaye ni mfungwa wa kifungo cha maisha ambaye pia ni nyapara Bw.Samweli Sanyage amekuwa akiwaonya  katika mahubiri yake mara kwa mara wafungwa na mahabusu kuacha kabisa mchezo huo.

Mkuu wa Gereza la Ruanda Dk. Malewa katika mikutano yake ya wafungwa na mahabusu amejitahidi kuwaonya mara kwa mara amekuwa akisema kesi nyingi zimekuwa hazimfiki.

Katika hotuba moja ya Agost,21,mwaka huu akizindua jezi za mchezo wa miguu ambapo ulifanyika mchezo baina ya mahabusu na wafungwa ambapo Dk.Malewa alisema kuwa michezo ni furaha na kwamba waache tabia ya kuingiliana na wajiadhari na ugonjwa wa ukimwi.

Dk.Malewa aliwaomba mahabusu na wafungwa kupima kwani dawa za kurefusha maisha zimeshafika Gerezani na kwamba kupima kunasaidia kuwa na uhakika na afya   na iwapo umeathirika usije ukamwambukiza mkeo pindi utakapo achiwa huru.

Mfungwa mmoja ambaye pia ni mmojawapo wa manyapara  Bw.Ahmed Dege katika mkutano mmoja alimuomba Mkuu wa Gereza kuingiza na kuruhusu kondomu zitumike ndani ya Gereza kwa kujikinga na maambukizo ya Ukimwi kwa madai kuwa vitendo vya ngono vimekithiri.

Ingawa Mkuu wa Gereza alijibu kuwa kuingiza kondomu ndani ya jela ni sawa na kosa la jinai, naye Mganga wa zahanati ya Gereza la Ruanda Bw. Oswald Hyera aliongezea kwa kusema kuwa  jitihada za kutoa elimu juu ya vitendo hivyo itaendelea kufanyika.

 Lakini bado kuna wafungwa na mahabusu wanaojali afya zao kwa kutumia kinga ya kondomu kama nilivyowahi kushuhudia mei,14 mwaka huu mfungwa mmoja jina namuhifadhi akifanya biashara ya  kuuza  kondomu moja aina ya salama kwa pande mbili.

Pia Januari,11 mwaka huu majira ya saa 4.30 asubuhi Nyapara mmoja wa Kifungwa alipokua akipekuliwa na ofisa mmoja wa Magereza mwenye cheo cha sajenti baada ya kutoka kufanya kazi za nje ya Gereza alikutwa na salama kondomu mbili kwenye ndoo ya plastiki.

Katika ukaguzi maalumu uliofanyika Septemba ,8.2004 Ofisa mmoja wa Magereza mwenye cheo cha nyota mbili aliokota  pakiti nne za kondomu aina ya salama zikiwa zimedondoshwa ardhini.   


Naye mahabusu mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Kyando alisema kuwa Serikali kwa kiasi Fulani inachangia kuongezeka kwa maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi kutokana na  kuwaweka mahabusu muda mrefu bila sababu za msingi hali inayopelekea wake zao kushawishika kujihusisha na vitendo vya ngono ili kujaribu kupambana na makali ya maisha.

Uchunguzi umebaini kuwa iwapo Polisi wangetumia vizuri sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai (CPA) ya mwaka 1985 inayowapa wakuu wa vituo vya polisi uwezo wa kutoa dhamana kwa watuhumiwa wa makosa madogo madogo kama wizi wa kuku na uzururaji ingeweza kupunguza msongamano na hivyo kupunguza vitendo vya kulawitiana magerezani.

Kwa mujibu wa Kifungu cha 6(1) cha sheria no.7 ya mwaka 2001 ya tume ya haki za binadamu kinaipa tume mamlaka ya kutembelea na kukagua magereza lakini tume haijapita katika Gereza la Ruanda takribani mwaka mmoja  tokea Juni,2004 hadi Septemba,30.2005.

Ni maoni yangu kuwa taasisi zinazojihusisha na haki za binadamu zitembelee magereza mara kwa mara na wasiridhike na taarifa za  Wakuu wa Gereza wa Mikoa, (RPO) ama  wasiishie maofisini.


Pia Viongozi na Taasisi husika  mnapotembelea magereza sikilizeni maoni ya wafungwa na mahabusu moja kwa moja  vile vile watumishi wa  Taasisi hizo waingie magerezani kama mahabusu ili kufanikisha kufanya uchunguzi wa kina.

Magereza pia izangatie sheria na haki  za mikataba ya umoja wa Mataifa kuhusu hifadhi ya haki za binadamu na wajibu kwa jamii kwa mahabusu na wafungwa magerezani.

Watendaji hao wanapaswa kutambua kwamba haki za msingi za binadamu huathirika kwa kiwango kikubwa mtu anapotiwa Gerezani kwani uhuru wake uathirika,utu wake huchujuka na haki zake za msingi hukandamizwa

Idara ya upelelezi wa makosa ya jinai pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu zisicheleweshe kesi zikamilishe upelelezi kwa muda muafaka ili kuondoa mlundikano Magerezani na kwamba njia nyingine za adhabu zitumike mathalani wafungwa wanaotumikia adhabu ya vifungo chini ya miaka mitatu wapewe adhabu za faini, adhabu ya huduma kwa jamii.

Lakini pia waTanzania jifunzeni kuishi kwa amani,  utulivu na kufuata maadili mema,tafuteni njia mbadala zinazokubalika katika kujipatia riziki,rizikeni na kile mnachokipata na fuateni taratibu na sheria za nchi zilizowekwa.

Inaendelea…

No comments:

Post a Comment