Tuesday, March 29, 2011

makala-maisha ya gerezani na uozo unaofukuta


Na Thompson Mpanji,


KUNA msemo usemao “Ukistaajabu ya Mussa utayaona ya Firauni”. Naukumbuka na kuuwaza msemo huu kila nikumbukapo mambo niliyoyashuhudia na baadhi kusimuliwa kuwa yamekuwa yakitendeka ndani ya gereza maarufu mkoani Mbeya, gereza la Ruanda.

Kwa wale ambao wamekuwa wakiishia kusoma masimulizi ya Sodoma na Gomora katika masimulizi ya vitabu mbalimbali vya kale, bilashaka wanaweza kuwa wamepata sehemu ya kuyashuhudia masimulizi hayo kwa macho yao kwa kushuhudia yanayojiri ndani ya gereza hili kongwe nchini.

Ni gereza ambalo pia litakukumbusha pia juu ya zile simulizi za samaki wakubwa kuwala samaki wadogo, tena kwa kutumia kila aina ya hila ili kutimiza malengo yao. Ukaifanikiwa kuingia ndani ya Ruanda, bilashaka utastaajabishwa na harakati, mbinu na kila aina ya hila ambazo hufanywa na binadamu (wafungwa kwa mahabusu)  za kutaka kulana bila soni wala huruma.

Nilipokuwa nikisoma vitabu mbali mbali vya dini vilivyokuwa vikielezea mambo ya Sodoma na Gomora, nilikuwa nikidhani kuwa ni hadithi tu, na nilipokuwa nikisikia juu ya uwepo wa watu wenye kushiriki matendo ya Ki-sodoma na Gomora, katika zama hizi, wakiwemo wanaume mashoga au wanawake wasagaji, bado ilikuwa hainiingii akilini.

Lakini ndugu yangu baada ya kukumbwa na mkasa ulionipelekea ‘niswekwe’ ndani ya gereza hilo, ambalo wenyeji wake (wafungwa wazoefu), wanaliita ‘Kigali’ wakiwa na maana mji mkuu wa nchi ya Ruanda,  nilyoyakuta huko yalinifungua kabisa macho na kunifanya nijione kama niko dunia nyingine na sio hii niliyokuwa nimeizoea.

Namshukuru Mungu sio tu kwa kuwa niliingia na hatimaye kutoka katika gereza hilo nikiwa mzima kiafya, bali pia kwa kuniepusha na tamaa ya kuliingia balaa hili la kujihusisha na biashara hii ya kishetani.

Si nia yangu kuwaelezeni juu ya kile hasa kilichosababisha mimi kujikuta niko Kigali, baada ya kukumbana na maafande wetu ambao ustaarabu kwao ni msamiati ambao hawakuwahi kujifunza katika maisha yao ya kusoma, bali zaidi kuwaelezeni kwa lengo la kuwaelimisha juu ya hali halisi ya kilichopo ndani ya gereza hili, kitu ambacho naamini kabisa ndicho kinachopatikana katika magereza yetu yote hapa nchini.

Kimantiki, magereza huwa ni sehemu ambazo hupelekwa watu ambao kwa namna moja ama nyingine wanakuwa wameshindwa kabisa kuendana na misingi au taratibu za kijamii za kimaisha, ikimaanisha kuwa magereza ni sehemu ambayo mwanadamu hutakiwa kwenda kujifunza ustaarabu kisha arejee katika jamii. Ndio maana hata jirani zetu Zanzibar sehermu hizio huziita Vyuo vya Mafunzo.

Hata hivyo katika Tanzania, jambo hili ni kinyume kabisa. Katika gereza la Ruanda kwa mfano, niliyashuhudia mengi ikiwa ni pamoja na jinsi mwanaume ‘anavyomsulubisha’ mwanaume mwenziye kinyume cha maumbile bila ya huruma.

Katika sehemu hii kikubwa ambacho kinachofundhwa kwa jamii iliyokusanywa hapo kwa lengo la kubadilishwa mawazo ni suala la kulawitiana, kiasi cha hata baadhi ya raia wa sehemu hizi kuwa wengine wamefikia hatua ya kuoana. Kuoana wanaume kwa wanaume? Hiki ndicho kinachofundishwa hata kwa wale ambao walisingiziwa na kukumbwa na balaa la kuswekwa ndani.

Ukimuuliza huyo ‘mlaji’kuwa ni kitu gani kinachompelekea kujizira kiasi hicho atakujibu uache kumfuatilia kwasababu wanawake hawapo humo gerezani  wataishije na namba (kifungo) ni ndefu? wakati huo anakuonesha  namba yake ya kifungo ambayo inaonesha anatoka mwaka 2040, hiyo ndiyo sababu wanayoiona ni ya msingi kwao.

Sasa unabaki kujiuliza kwanini mtu huyu hasivumilie na kujitunza ili pengine aweze kuishi kwa muda mrefu zaidi na pengine msamaha unaweza ukampitia na akaachiliwa  huru akiwa salama.

“Mimi hivi sasa nina umri wa miaka 55 na nimepewa adhabu ya kutumikia kifungo cha miaka 45,ebu fikiria kama kweli nikibahatika kutoka si nitakuwa sina nguvu kabisa kama sio kufia humu humu, kwanini nisimalizie nguvu humu humu jela?” alisema mfungwa mmoja ambaye alidai kuwa ana ‘watoto wa kijelajela’wanne.

Kwa wale wasiojua misemo ya magereza, Watoto wa kijelajela humaanisha sawa na wanawake huku uraiani, ikimaanisha kuwa mfungwa huyo yeye anawake wane hapo gerezani.

Mfungwa huyu ambaye jina namhifadhi, katika masimulizi yake kwangu, aliendelea kusema kuwa vijana wenyewe wanajipeleka kutokana na shida zao mbali mbali. Wapo wanaojiingiza katika matendo hayo kutokana na kutokutosheka na mgao wa kawaida wa chakula, wapo wanaotaka kupata sigara, unga,  bangi na wapo ambao hutaka kuvaa vizuri na kwamba yeye  huduma hizo zote anazimudu kuwatekelezea.

Pia imebainika kuwa maandalizi mabaya wa chakula  ambacho pia hakitoshi (pungufu ya gramu 500) kukidhi njaa kwa mahabusu na wafungwa ni sababu mojawapo inayochangia kuenea kwa tabia hii ya kulawitiana.

Kwa upande wa vyakula, magereza kuna utaratibu wa aina mbili. Kwanza kuna sufuria linalopikwa kwa ustadi wote ambalo linakuwa ni maalum kwaajili ya wapishi na malwatani ambao kiwango chao cha kawaida cha chakula, iwe ugali au chakula chochote huwa ni zaidi ya mara nne ya mgao wa kawaida wa wafungwa gerezani. Sio jambo la ajabu kumkuta mfungwa wa aina hii akiwa na ugali zaidi ya  gramu 2000 ulio mzuri na ulioiva. Pia  maalwatani hao wanakuwa na Mboga tofauti tofauti (samaki wabichi, mboga za majani, mayai na nyama)  iliyokaangwa kwa mafuta.

Aina ya pili ya vyakula ndani ya gereza hili kama ilivyo katika magereza mengi ni ile ya vyakula vya walalahoi ambao hupokea  ugali mbichi dirishani usiofikia hata gramu 500 pamoja na mboga yenye ujazo wa gramu 30 iliyochanganywa mchicha, maharagwe na dagaa bila kusahau konokono wadogo na michanga bila mafuta.

Nafikiri kutokana na hali hiyo utakubaliana na mimi kuwa hapo inawezekana kabisa ‘samaki mkubwa akammeza kwa urahisi samaki mdogo pasipo shaka yeyote na kwamba  chakula kuwa kidogo ndiyo sababu mojawapo inayopelekea watu kushawishika kujihusisha na vitendo hivyo.

Lakini pia kwa wale wenzangu  ‘machain smoker’ ambao wanapenda kuvuta sigara ama bangi wanakamatika kwa urahisi na kushawishika na vitendo hivyo na watu wa aina hiyo  wengi wao wamekuwa radhi kufanya vitendo hivyo vichafu kwa minajili ya kuwa na uhakika wa kuvuta kila siku.

Bei ya sigara moja iwe sportsman, sweet menthol ama club na kadhalika ni mapande mawili ya sabuni ikiwa na maana sh.100/- kwa maana kipande cha sabuni ya kufulia ambacho huku uraiani kinauzwa sh.100/- kwa jela thamani yake ni sh.50/- ambapo tumbaku au ‘Mbama’ kwa lugha maarufu ya jela inauzwa pande moja.

 Wapo watu wenye uwezo wa kuwagharimia kiasi cha sh.500/- kila siku watoto wao kwa ajili ya uvutaji mbali ya kuwanunulia matunda, vitafunwa kama chapati, maandazi ama kinywaji kama juisi za kwenye vipakiti..

Malazi ni moja ya sababu kuu inayowafanya watu washawishike na kukubaliana kulegeza masharti ya msimamo mkali wa kutojihusisha na biashara hiyo kwa mfano tukiachia vilago vilivyoishia Septemba,2004 na kuletewa godoro za sponji zenye urefu wa nchi sita na upana inchi mbili na nusu.

Godoro hizo zimewekwa 32 katika kila chumba cha kulala chenye urefu wa futi 40 na upana wa futi 15 lakini watu wanafikia kulala (kwa mfano novemba,28.2004 walilala watu  94,februari,2.2005 walilala watu 102) katika chumba kimoja  wakati huo huo kuna manyapara wa kifungwa watano katika kila chumba ambao wao kila mmoja analala katika godoro lake.

Mbali ya hao viongozi wa kifungwa kuna maaskari wa chumba cha kulala (maaskari cell) ambao wanakuwa watatu katika kila chumba cha kulala ambao nao kila mmoja anakuwa na godoro la peke yake la kulala na pia  viongozi hao wote wanakuwa na magodoro ya ziada kwaajili ya ndugu jamaa,’Warombo’ (yaani watu wanao ishi nao kwaajili ya manufaa fulani) pamoja na‘watoto wa kijelajela’.

 Kwa wastani jumla ya  godoro 16 zinakuwa zimeshamilikiwa na hivyo kubakia godoro 16 ambazo watu  watalundikwa hapo  panapoitwa kichakani au sensa kwa hiyo karibu watu 64 wanatakiwa walundikwe katika godoro16 zenye upana wa inchi mbili na nusu.

Ni matumaini yangu utakuwa umeshapata picha halisi ya ulalaji ndani ya jela   kiasi kwamba watu wanalazimika aidha kwa lazima ama kwa ridhaa yao wenyewe kucheza mchezo huo wa kishetani.

Kutokana na hali hiyo ndiyo maana kesi za ‘kunyatiana’kuingiliana bila ya ridhaa zinakuwa nyingi, japo huku uraiani hazisikiki mara zote.

Mfano kuna kesi ya wafungwa kunyatiana iliyotokea Januari,3.2005 ambapo mnyatiaji alipewa adhabu ya kufungwa pingu mikononi na miguuni kwa muda wa siku saba na baadaye alihamishiwa Gereza la kilimo la Songwe lililopo Mkoani hapa.

Lakini pia wapo watu wanaolazimika  kujiingiza katika biashara hiyo kukwepa ‘harasi’ za mara kwa mara kwa kupigwa na hao viongozi (Nyapara) na kusingiziwa sababu za uongo kwa maaskari jela kama vile kuwa na fedha ukapigwa kirungu mpaka uoneshe ulipoficha, umechukuwa chakula mara mbili wakati siyo kweli, ama utakuwa unachaguliwa kila wakati kufanya usafi na pia utakuwa unanyimwa maji hata ya kuoga.

Hiyo yote ndiyo mitego wanayoitumia wataalamu hao kuwanasa ‘watoto wa kijela jela na hatimaye kuwaweka katika himaya zao na kuwatumia kadri wapendavyo.

Pia wapo wale ‘watoto wa kijela jela’ wazoefu ambao wao  wamekubuhu katika fani hii hawa huwa hawana ‘wazee,’ wao huwa wanafanya mchezo wao wa chapu chapu  sehemu ya vyoo maarufu kama machemba na kumaliza shida yako kwa makubaliano ya pande nne za sabuni,10 ama 20. 

 Uchunguzi wa kina umebainisha kuwa huko chooni biashara hiyo huwa inafanyika muda wa mchana wakati mahabusu wanaenda kula na ndipo utakuta mwangalizi wa choo anaanza kufanya usafi wa kupiga deki na kuweka mpira wa kuzibulia kinyesi mlangoni (maarufu kama mchokocho) ikiwa ni ishara ya kutoruhusiwa mtu kuingia kwa muda huo ama kunakuwepo mtu anayezuia watu wasiingie kwa kisingizio cha kufanya usafi wakati siyo kweli.

Aidha imebainika kuwa vijana wanaoongoza kwa kujihusisha na vitendo hivyo ni pamoja  na vijana wa makabila wa Kinyiha wakifuatiwa na Wamalila, Wasangu na Wanyamwanga  na hii inatokana na wengi kutoka katika vijiji vya mbali na hivyo kuwa ni rahisi kudanganyika  ama kutishiwa.

Pia kanuni ya viwango vya kimataifa ya kuwatenga watoto na watu wazima haifuatwi katika gereza hili hali inayopelekea watoto kutomudu misukosuko ya vitisho vya kibabe na badala yake  kuishia kujiingiza katika biashara hii haaramu na hatari kwa pande ziote zinazohusika.

Kulikuwa na matukio mawili kwa mfano ambayo yalihusisha watoto walioshurutishwa na uzembe wa serikali yetu kutupia macho magereza na sheria za kimataifa za magereza kwa watoto ambapo katika tukio la kwanza mtoto mmoja wa miaka 13, aliyekuwa mahabusu Oktoba, 8.2004 alidaiwa kulawitiwa mara mbili na Nyapara mmoja.

Tukio hili lilikuja kubainika Oktoba18,2004 baada ya Mganga wa zahanati ya Gereza Dk.Oswald kuthibitisha, lakini kesi hiyo haikufika kwa Mkuu wa Gereza iliishi mikononi mwa Manyapara wa Kifungwa.

Katika tukio jingine Nyapara mwingine wa kifungwa alivuliwa cheo hicho na kuhamishiwa katika Gereza la Ileje kutokana na kumlawiti kwa nguvu na kumsababishia maumivu makali kijana mmoja mkazi wa Uyole mkoani Mbeya.

Hata hivyo Wanafunzi wawili ambao waliingia katika Gereza hilo kwa kutuhumiwa kuiba sh.40,000/- za wazazi wao walijutia kuingia kwao Gerezani kutokana na kutokuwa wasikivu kwa wazazi wao.

Vijana hao mmoja ana umri wa miaka 16 mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya Sekondari ya Mbeya Day na mwingine mwenye umri wa miaka 17 mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya Sekondari ya Igawilo ambao waliingia Gerezani Septemba,7 mwaka huu  walisema kuwa walisumbuliwa sana kwa nia ya kuwataka kimapenzi.

Inaendelea.....

No comments:

Post a Comment