Na Thompson Mpanji,Chunya
Katika kusherehekea siku kuu ya wafanyakazi mei mosi ambayo kitaifa ilifanyika mjini Morogoro,ambapo mgeni rasmi alikuwa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania,Jakaya Kikwete,huko wilayani Chunya kuna taarifa ya Waziri mmoja kuhitimisha shamra shamra za sherehe hizo kwa kupata kikombe kutoka kwa mlemavu wa macho.
Akiongea na mwanablog hii Mkazi wa Kijiji cha Mbuyuni,Bw.Nico Haule amesema Naibu Waziri wa elimu na mafunzo ya ufundi,Mh.Philipo Mulugo jana alikuwa miongoni mwa wananchi waliokwenda kupata tiba ya kikombe kutoka kwa mpiga kura wake Mlemavu wa macho,Bw.Simon Mahela aliyedai kuoteshwa na babu yake marehemu kutibu magonjwa yote sugu ikiwemo na ukimwi kwa muda wa siku 43.
Bw.Haule ambaye pia ni mdau wa masuala ya habari,amesema Bw.Mulugo ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Songwe alikuwa mgeni rasmi katika sherehe za mei mosi ambazo zilifanyika Chang’ombe,Kata ya Mbuyuni,wilayani Chunya ambapo baada ya kuhitimisha sherehe hizo kwa kutoa msaada wa Sh.200,000 ili kusaidia shughuli za mei mosi ziweze kuendelea yeye na makatibu wake wa jimbo walikwenda kushuhudia tiba hiyo na hatimaye kupata kikombe cha tiba na hivyo kukonga nyoyo za wapiga wake na kumuona ni mwenzao.
Mlemavu huyo wa macho anatoa tiba hiyo kwa masharti ya matamio ya siku 43 bila kunywa pombe wala kufanya tendo lolote la ndoa amekuwa akitoa huduma kwa familia nzima kuchangia sh.500 ambapo siku ya Ijumaa watoto na wanafunzi wanakunywa kikombe bure.
Hata hivyo Bw.Haule amesema viongozi kadhaa wa Wilaya ya Chunya akiwemo Mkuu wa Wilaya hiyo, Bw.Deodatus Kinawiro ameshafika kupata tiba ya mlemavu huyo wakati alipokuwa katika ziara za kikazi.
Mwisho.